'SIMBA SC. HONGERENI NA KILA MTU AWAJIBIKE KWA NAFASI YAKE'
Dar es Salaam
SIMBA SC ni klabu kongwe ambayo watu wengi
wanategemea ipate mafanikio waka wowote, lakini msimu wa mwaka jana na msimu
huu imesuasua sana na kuwanyong`onyesha mashabiki wake waliokuwa na matarajio
makubwa na kikosi chao.
Katika maisha ya kawaida, kuna wakati mambo
yanakuwa safi na kuna wakati mambo yanakuwa magumu.
Kipindi cha mpito huwa kinatokea, na ndio maana kuna
muda unaweza kuwa na pesa nyingi na kufurahia maisha, lakini ikafika wakati
ukakosa hata mie moja.
Kimsingi inapotokea hali mbaya kwako ndio kipimo
chako, na jamii itahitaji kuona jinsi unavyokabiliana na changamoto yako.
Mtandao huu ulifanya mahojiana na katibu mkuu wa
Simba sc, Ezekiel Kamwaga ambaye kwa asilimia kubwa ndiye mtendaji mkuu wa
shughuli zote za klabu.
Katika mahojiano hayo, Kamwaga aliwatoa hofu
mashabiki wa Simba kuwa klabu haina mgogoro wowote baina ya benchi la ufundi na
wachezaji, au viongozi na benchi la ufundi au viongozi na wachezaji.
Kamwaga alibainisha kuwa hali iliyowatokea Simba
katika misimu miwili mfufulizo ni matokeo ya kimpira kwani wakati fulani upepo
mbaya unaweza kuvuna kwa klabu yoyote.
Pia alisema hali kama hiyo inaweza kuipata klabu
yoyoye katika mpira.
`Mr. Liverpool` aliitolea mfano klabu yake ya
Liverpool inayoishabikia kuwa imekaa miaka 24 bila kutwaa kikombe.
Pia alisema kwasasa Manchester United imekuwa katika
wakati mgumu zaidi, lakini hawana sababu ya kushuka morali.
Kamwaga alisema kama klabu kubwa namna hii huwa
zinapitia wakati mgumu, basi ni fundisho hata kwa Simba.
Wakati Kamwaga akizungumza hayo, nilikuwa na shauku
kubwa ya kusikia sasa wanafanyeje baada ya kuwa katika hali ngumu.
Mosi; niligundua kuwa Simba wamekubaliana na
matokea. Katika maisha ya soka, kukubaliana na kile kinachotokea uwanjani ni muhimu sana. Mpira huwa una
kupanda na kushuka.l
Klabu inaweza kuwa bora na ikasheheni nyota wakubwa,
lakini ikashindwa kufikia malengo yake.
Nilishawasikia makochwa wengi wakiwemo akina Pep
Guardiola, Jose Mourinho, Alex Fergusons na wengine wengi wakisema kuwa
hawaelewi kwanini wamepoteza mechi.
Kocha anasema kwa asilimia nyingi timu yake
imemiliki mpira na kupata nafasi nyingi za kufunga, lakini imeshindwa kupata
ushindi.
Mfano timu inapata nafasi saba za wazi, lakini
inashindwa kutumia hata moja. Timu pinzani inapata nafasi moja inafunga na kushinda
bao 1-0.
Kocha anaibuka na kusema timu bora imepoteza mchezo.
Timu yake ilikuwa bora kwa idara zaole, lakini wamefanya kosa moja na kufunga.
Kumbe kuna wakati mpira huenda na bahati uwanjani.
Hili la Simba sc kukubali kuwa matokeo wayapatayo
uwanjani ni ya kimchezo, ni hatua nzuri.
Mengi yamezungumzwa
kuwa Simba kuna mgogoro baina ya viongozi na wachezaji, na wakati fulani
ilisemwa kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, Zdravko Logarusic hana mahusiano mazuri
na wachezaji wake.
Sababu nyingi zilitolewa ni kuwa kocha huyo ni mkali
mno kwa wachezaji wake, hivyo wanapocheza wanahofia kukosea na kutolewa.
Lakini kuna wakati liliibuka suala la kuchelewesha
mishahara na posho kwa wachezaji.
Hapa yalisemwa mengi na wengine wakafika mbali na
kusema mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage ameshindwa kuendesha klabu.
Kama kweli wachezaji wanacheleweshewa haki yao, ni jambo
mbaya kwasababu linaweza kuwaathiri kiutendaji.
Inapotokea kiongozi wa juu wa Simba, Ezekiel Kamwaga
na kuusemea uongozi wake kuwa hakuna mgogoro wowote ndani ya klabu bali ni
matokeo tu, basi ni jambo jema katika kukabiliana na tatizo.
Hakuna haja ya kushikana uchawi, ilimradi wamekubali
ukweli, basi ni jambo la kukaa chini na kutafuta mwarobaini wa tatizo lao. Kwahili naipongeza Simba sc.
Simba sc baada ya kukubali matokeo,
wamezungumzia jambo la pili na la msingi la mashabiki wao kutokataa tamaa na
kuendelea kuiunga mkono timu yao.
Kamwaga aliwatoa mashabiki wa Simba na kuwataka wawe na imani na wachezaji wao, benchi la ufundi na uongozi wao.
Mashabiki wa mpira ni mchezaji wa 12 uwanjani.
Hakuna kocha wala kiongozi anayeweza kudharau
mchango wa mashabiki katika maendeleo ya Soka na Klabu.
Mashabiki ni msingi imara wa kufikia mafanikio kwasababu
ni washauri wazuri na wanajenga morali kwa wachezaji wanapokuwa uwanjani.
Kuna raha kubwa kwa mchezaji anaposakata kabumbu na
kusikia makelele mengi ya kumshangilia kwa kazi yake nzuri aifanyayo uwanjani.
Na ndio maana kumzomea mchezaji kunaweza kumpunguzia
ufanisi wake hasa kama hajajengwa kisaikolojia kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa hiyo mashabiki ni muhimu sana katika mpira. Kwa
kutambua hilo, uongozi wa Simba unawaangukia mashabiki wake, hasa katika wakati
huu mgumu walionao.
Kama ni
shabiki wa kweli, huna haja ya kususia kwenda uwanjani kwasababu ya timu yako
kukosa matokeo mazuri mechi za nyuma.
Lazima uendee kutoa mchango kwa nafasi yako ili
kuifanya timu ijikwamue katika mazingira magumu.
Ipi ni sababu ya mashabiki wa Simba kupunguza kujaa
uwanjani? Sidhani kama kuna nyingine zaidi ya matokeo mabaya kwa klabu.
Kamwaga anaposema mashabiki wasiwe na hofu na
waendelee kuiunga mkono timu yao, basi mashabiki wa Simba wamsikie kiongozi wao
na kubadili fikira zao kuelekea michezo miwili ya kufunga msimu.
Kuwakalisha mashabiki wao na kuwaomba waendelee kuwa
karibu na timu ni hatua nyingne ya pili kwa Simba kutatua matatizo yao.
Nawapongeza kwa hili pia.
Tatu; Simba sc wameonesha kuwa na mipango ya
kuimarisha kikosi chao baada ya kushindwa kutamba kama miaka ya Nyuma.
Kamwaga alisema kwasasa timu inajiandaa na mchezo wa
jumamosi dhidi ya Ashanti United ndani ya uwanja wa Taifa.
Baada ya mechi hiyo watakuwa wanajiandaa na mechi ya
mwisho dhidi ya Yanga aprili 19 mwaka huu.
Hii ni mechi muhimu ambayo pengine inaweza kuleta
umoja miongoni mwa wana Simba.
Kuna raha kubwa kwa Simba kuifunga Yanga au Yanga
kuifunga Simba sc.
Mechi baina ya timu hizi huwa hazitabiriki hata
kidogo na huwezi kutumia sababu ya timu moja kuwa na kikosi kizuri kusema
itaifunga timu nyingine.
Mambo huwa yanabadilika kabisa na timu ya kawaida
inaweza kupambana na kila mtu akabaki, ooh! Walikuwa wapi mechi za nyuma
kucheza kama hivi?.
Kwa kutambua hilo, uongozi wa Simba umeanza mikakati
ya kuelekea mechi hiyo kwa malengo ya kulinda heshima.
Baada ya mechi hiyo, Kamwaga alisema watakuwa na
kikao kizito cha viongozi wa timu hiyo kujadili matatizo yaliyowasibu msimu
huu.
Hapa wanatarajia kubaini mapungufu na makosa
waliyoyafanya na kuambulia walichovuna msimu huu.
Bila shaka lengo la kikao hiki ni kutafuta njia ya
kuboresha timu na si kushikana uchawi.
Kamwaga alisema msingi wa kikao hicho utajengwa
kupitia ripoti ya benchi la ufundi.
Bila shaka Logarusic na Matola wana sababu nzuri
zaidi ya mtu yeyote juu ya sababu za Simba kufanya vibaya.
Wao ni makocha na wanakaa na wachezaji wao kwa muda
mwingi, hivyo kutumia taaluma yao wanafahamu kwanini Simba inapata matokeo
mabaya.
Ripoti yao
itabainisha mapungufu ya kikosi na nini kifanyike ili kubadili hali ya hewa
msimbazi.
Sina hakika kama watakuwepo, lakini nadhani bado
uongozi wa Simba unawaamini makocha wao na watawapa nafasi nyingine.
Simba wanahitaji kutuliza akili katika kikao hiki
ili wapate mwarobaini wa tatizo lao.
Kama watahitaji kusajili wachezaji wengine ili
kuimarisha kikosi chao, basi litakuwa wazo zuri, lakini walimu waachiwe mpango
huo.
Yupo Logarusic, Matola, Basena na watu wa kamati ya
ufundi ambao wanao uwezo wa kutafuta wachezaji wazuri.
Masuala ya viongozi wasiohusika na mambo ya ufundi
kuingilia usajili, itakula kwao na watashindwa kufikia malengo yao.
Cha msingi uongozi na kamati ya usajili
inayoendeshwa na kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
Zacharia Hans Poppe, kazi yao pekee iwe ni kusainisha mikataba wachezaji
waliochaguliwa na makocha wao.
Itakuwa jambo bora zaidi kuwaachiwa makocha wasajili
wachezaji wanaowataka na kuwaacha wanaoona hawana faida kwa timu.
Makocha wanazunguko katika mechi 26 wakiongoza
vikosi vyao. Wanawafahamu wachezji wao na kuwaona wachezaji wa timu nyingine,
hivyo wanajua nani anawafaa na nani hawafai.
Wakiwaamini walimu hawa, wanaweza kuleta mabadiliko
makubwa katika klabu.
Nawapongeza Simba kwa mambo haya matatu niliyosema
hapo juu ambayo kwa kifupi ni kukubali matokeo, kuwatoa hofu mashabiki na
kuwataka waendelee kuiunga mkono klabu yao na tatu ni kuwa na mipango ya
kuboresha kikosi chao kwa msimu ujao.
Kuishia nafasi ya nne kwa timu kama Simba, lazima
inaumiza roho za mashabiki wengi waliopo nyuma ya klabu.
Kila mtu kwa nafasi yake akubali kuwajibika ili
kufikia malengo yao.
Kila la kheri Simba sc katika mikakati yenu ya
kuimarisha kikosi chenu ili Simba ya zamani urudi ulingoni.
Comments
Post a Comment